April 1, 2016



Na Saleh Ally
UKIZUNGUMZIA suala la ubora wa wafungaji katika Ligi Kuu Bara, hautaweza kukwepa kuwataja washambuliaji wageni kuwa ndiyo bora.

Nafasi ya kwanza hadi ya tatu, sasa inashikiliwa na wachezaji kutoka nchi nyingine, si hapa nyumbani Tanzania.

Hamisi Kiiza wa Uganda anayeichezea Simba anaongoza kwa kuwa na mabao 19, anafuatiwa na Amissi Tambwe kutoka Burundi mwenye 17 na Mzimbabwe Donald Ngoma yuko katika nafasi ya tatu.

Baada ya hapo, wa kwetu, yaani Tanzania nao wanaanza kuonekana. Wa kwanza ni mshambuliaji nyota wa Prisons, Jeremiah Juma mwenye mabao 11, halafu Mtanzania tena Elias Maguri mwenye 10 na mzalendo mwingine, Ibrahim Ajib mwenye mabao tisa sawa na Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast anayekipiga Azam FC.

Niwe mkweli, pamoja na kuona wafungaji wanachuana kwa kasi kubwa. Kwanza huwa nina majonzi lakini bado nafurahishwa na hali hiyo.

Kwamba timu ambazo zimesajili washambuliaji watatu wa juu yaani Yanga wenye Tambwe na Ngoma na Simba mwenye Kiiza wana kila sababu ya kuona walikuwa wanapatia kwa kuwa wanakwenda vizuri na wanaonyesha maana ya kuwa na washambuliaji kutoka nje ya Tanzania.


Naumia sababu ya uzalendo, kwamba vipi vijana wa nyumbani mbona wako mbali sana? Wanaanzia nafasi ya nne kwenda chini tena wakiwa wanazidiwa mbali na aliye katika nafasi ya kwanza.

Tatizo lao kubwa ni lipi hasa, vipi wanashindwa kuuthibiti au kuufikia ushindani kama ambao wanauonyesha wapinzani? Kwani kipi wanakosa ambacho kinawaondoa kwenye reli kiasi hicho?

Mtu anayeweza kuwa mfano ni Maguri, mshambuliaji tegemeo na hatari wa Stand United aliyekuwa na mabao 10 tangu mzungumko wa kwanza na sasa ni zaidi ya mechi sita au saba hajafunga hata bao moja.

Maguri ameshindwa kuendeleza makali aliyoyaanzisha mara baada ya kutua Stand United huku Simba wakiona hakuwa na lolote la ziada, ghafla akadorora, baadaye ikazoeleka kwamba hafungi tena na sasa ni zaidi ya kawaida.

Maguri amekuwa akizungumza kuhusiana na kocha wake, Patrick Liewig kutaka kuonyesha yeye ndiye chanzo cha yeye kutofunga. Tena mara kadhaa amekuwa akilaani kwamba Liewig hamchezeshi.

Ajabu ni kwamba hata pale alipomchezesha, bado Maguri hakuwa na msaada hasa katika ufungaji. Sasa katika hali ya kawaida unaweza kusema ni yupi hasa mwenye tatizo?

Jukumu la kufunga ni lake Maguri, kama kocha anampanga lazima afanye hivyo au kutoa msaada mkubwa. Ushauri wangu aache kulaumu kuhusiana na Liewig, badala yake awekeze nguvu kwenye kufufua juhudi za kusaka ufungaji bora.

Kiiza aliye kileleni anamzidi Maguri mabao tisa, Tambwe anamzidi mabao saba na Ngoma anamzidi mabao tatu. Jeremiah ambaye ni Mtanzania mwenzake anamzidi bao moja.

Maguri ndiye alikuwa kinara, alikuwa akiwazidi wote hao walio juu yake. Ushauri wangu kwake sasa ni kuachana na hadithi za kuwa anabaniwa na Liewig na akipata nafasi ya kucheza, basi afunge. Kikubwa anachotakiwa kukumbuka ni kwamba hata alipofunga hayo mabao 10, Liewig alikuwa kocha wake Stand United, naye ndiye aliyempa hiyo nafasi.

Kama binadamu inawezekana kocha huyo amemkosea, lakini anachopaswa kufanya Maguri ni kuendelea kufunga mabao badala ya kuzungumza na kulumbana na mwalimu wake.

Kama ataona atakuwa ameshindwa kuelewana na Liewig, anaweza akaomba ‘njia’. Anachotakiwa kufanya katika kipindi hiki ni kufunga na kuisaidia Stand United.

Hadithi za Liewig, bado zinaweza zisiwe msaada kwake hata kidogo. Hivyo Maguri ana nafasi ya kuchagua, afunge akishindwa atafute nafasi sehemu nyingine afunge, maneno mengi hapana. 




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic